Dar/Dodoma. Moto wa kashfa ya ufisadi katika
akaunti ya Tegeta Escrow unaoendelea kuwaka bungeni, sasa unaonekana
kugeuka gharika inayoweza kuwakumba vigogo wengi zaidi na kuiweka
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika hali ngumu.
Kashfa hiyo ya uchotaji wa Sh306 bilioni za
akaunti ya Escrow, inahofiwa kuwakumba vigogo zaidi ya 50 ndani ya
Serikali wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu, wabunge, majaji na wakuu wa
taasisi za Serikali waliohusika.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa kutokana na
kuwapo kwa idadi kubwa ya mawaziri na watendaji wa Serikali na mahakama,
inatishia anguko la Serikali.
“Kuna waziri (anamtaja) ameniambia ameangalia ile
orodha ya watu wanaodaiwa kuchukua fedha hizo ni zaidi ya 52. Hofu yangu
hili jambo likiingia bungeni na kujadiliwa huenda likasababisha
kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri kwa mara nyingine,” alisema mbunge mmoja
kutoka Kanda ya Mashariki.
Wabunge wajipanga
Mbunge mwingine kutoka Zanzibar (CCM), alisema
kuwa anasubiri kwa hamu kuchangia katika mjadala huo ili waondoke wale
wote ambao wamekwapua fedha hizo.
Juzi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliitisha kikao
cha mawaziri ambacho kilihudhuriwa na baadhi ya mawaziri na walifikia
uamuzi kuwa suala hilo litajadiliwa ndani ya chama kabla ya kuingia
ndani ya Bunge.
“Kinachosubiriwa ni ripoti ya Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC) halafu tutakutana wabunge wa CCM kabla ya kwenda
bungeni,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Pamoja na hali hiyo, wabunge katika makundi
makundi kwa wiki nzima wamesikika wakijadili jambo hilo huku
wakilihusisha na mbio za urais mwakani.
Mbunge mmoja (jina tunalo) alisema kuhusishwa kwa
Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika sakata hilo kunatokana na mtuhumiwa
mmoja ambaye ni kiongozi katika Wizara ya Nishati na Madini, kuwa mmoja
wa meneja wake wa kampeni.
“Hakuna mahali ambapo Pinda ameguswa moja kwa moja
katika ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali)
wala Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), bali wanasema
ni kwa sababu ya kampeni za urais na mhusika mmoja katika sakata hilo
anatajwa kuwa kama Pinda akipata urais, yeye ndiye atakayekuwa Katibu
Mkuu Kiongozi,” alisema mbunge huyo kutoka upinzani.
Jana Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza
Mangungu akizungumza na gazeti hili, alisema sakata hilo linatakiwa
liishe kwa kuwa linaumiza uchumi wa nchi kwa kuwa mtambo wa IPTL ni
matatizo.

0 comments:
Post a Comment