Pages

  • Latest News

    Sunday, 24 May 2015

    NANI NI NANI URAIS 2015: Juma Duni Haji: Makamu Mwenyekiti wa CUF


    Juma Duni Haji ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) ngazi ya Taifa na ni Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar. Juma Duni alizaliwa Novemba 26, 1950, Zanzibar (Novemba mwaka huu anatimiza miaka 65).
    Alianza elimu katika Shule ya Msingi Mkwajuni mwaka 1959 hadi 1965 kisha akajiunga na Shule ya Sekondari Gamal Abdel Nassar (siku hizi inaitwa “Beit el Ras”) mwaka 1966 na kuhitimu mwaka 1969.
    Duni aliendelea na sekondari ya juu (kidato cha tano na sita) katika Chuo cha Lumumba, Zanzibar kati ya mwaka 1970–1971. Wakati akisoma Sekondari ya Beit el-Ras na Sekondari ya Lumumba, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa ASP.
    Duni alidahiliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma Shahada ya Sayansi katika Elimu (BSC Education) kati ya mwaka 1972 hadi 1975.
    Baada ya kuhitimu shahada ya kwanza, aliajiriwa kama mwalimu wa Sekondari ya Beit Al Ras, wakati huo ikiitwa Gamal Abdil Nassir (jina la Rais wa zamani wa Misri), na baada ya mwaka mmoja akahamishiwa Sekondari ya Lumumba na kufundisha kidato cha tano na sita na baadhi ya wanafunzi wake ni “magwiji” wa siasa za Zanzibar; Ismail Jussa, Thuwayba Kisasi na wengineo.
    Mwaka 1978–1979, Duni alikwenda masomoni Uingereza, akasoma na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Reading na aliporejea alihamishiwa Ofisi Kuu ya Wizara ya Elimu na kupewa wadhifa wa Ofisa Mipango ya Elimu.
    Duni alipata mafunzo mengine muhimu ya kitaaluma nchini Nigeria mwaka 1980 juu ya Mipango ya Elimu na mwaka 1982 alipelekwa Japan kujifunza kwa kina Mipango ya Kiuchumi.
    Pia, Mwaka 1980 Rais Aboud Jumbe, alimteua Juma Duni kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango (Zanzibar) na baadaye kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango (Executive Secretary Planning Commission).
    Duni alianza safari ya kisiasa kwa “kulazimishwa” mwaka 1984, baada ya serikali ya Muungano kutoa Waraka wa Serikali (white paper) na kutakiwa wananchi watoe maoni yao juu ya hali na matatizo ya Muungano.
    Makatibu wakuu wa Serikali ya Zanzibar ya wakati huo akiwemo yeye walitoa maoni dhidi ya muungano, uhuru huo wa kitaalamu uligeuzwa kuwa mchungu kwani walisingiziwa kwamba wamefanya kinyume na walivyoagizwa na baadhi yao wakapewa onyo kali na wengine wakateremshwa vyeo.
    Duni aliteremshwa cheo kutoka wadhifa wa Katibu Mkuu hadi mwalimu wa kawaida kwa Tangazo la Rais, akatakiwa kwenda kufundisha Shule ya Mikunguni.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: NANI NI NANI URAIS 2015: Juma Duni Haji: Makamu Mwenyekiti wa CUF Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top