MKE wa rais, Mama Salma Kikwete, amesema serikali inatambua na kuthamini kazi za wajasiriamali wa Tanzania na kuwataka waongeze juhudi katika ubunifu.
Akizungumza alipotembelea Banda la Pride, lililo mahususi kwa wajasiriamali wa kazi za ubunifu, Mama Salma alisema wajasiriamali wa nchini wanatambulika kutokana na kazi zao, hivyo ni vema wakaboresha.
Alisema kilichobaki ni kutambulika kimataifa na juhudi zinafanywa na serikali ili wajasiriamali waanze kuuza bidhaa zao nje ya nchi ikiwemo kukabiliana na changamoto za soko la Afrika Mashariki.
Mmoja wa wajasiriamali kutoka Morogoro, Lea Mwana, alisema tatizo wanalokumbana nalo ni watu wa Jamhuri ya China kuwaibia ubunifu wao na kutengeneza kazi zinazofanana chini ya kiwango.
“Sisi tunabuni, wao wanakuja wanachukua maua na mitindo yetu, mwisho wa siku wanaleta vitu vyao visivyo na ubora na kuuza kwa bei ya chini na kazi zetu zinaonekana za gharama na kuachwa, maana Watanzania wanapenda bidhaa za bei chini, hawaangalii ubora,” alisema.
Aliiomba serikali kuhakikisha wanapambana na ubora wa bidhaa na si kuachia soko huria liharibu bidhaa zao zenye ubora.
0 comments:
Post a Comment