KUTOKANA na mfumo wa kisoka duniani, Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA), limehakikisha kila nchi ina ligi kuu ya soka inayoshindanisha baadhi ya klabu katika nchi husika.
Aidha, kila ligi haikosi watani wa jadi ambao kwa namna moja ama nyingine hunogesha ligi hizo kiasi ambacho mashabiki huvutiwa kutaka kufuatilia kwa karibu kutokana na ile hali ya upinzani katika soka.
Ligi ya Afrika Kusini, kuna timu za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates, Hispania kuna Barcelona na Real Madrid, nchini Italia kuna AS Roma na AC Milan. Halikadhalika hali kama hii ipo pia katika ligi za Ufaransa na Uingereza. Hapa Tanzania kuna Simba na Yanga.
Wakati klabu za wenzetu zikipambana kwa kuonyesha kiwango cha soka ndani na nje ya nchi zao, hapa Tanzania hali ni tofauti. Ni kawaida kwa Simba na Yanga kujizolea sifa kubwa zinapozitesa klabu ndogo katika ligi ya nyumbani.
Mathalan, kwa sasa Klabu ya Yanga ndiyo inayong’ara baada ya kushinda mechi nyingi katika ligi, kama hiyo haitoshi wiki chache zilizopita wameitoa klabu ya Komorozone ya nchini Comoro katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika kwa jumla ya mabao 12-2.
Kama hiyo haitoshi Februari 22 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wameichapa klabu ya Ruvu Shooting kwa mabao 7-0. Vilevile Yanga imekuwa klabu ya kwanza kuvunja mwiko wa Mbeya City wa kutofungwa katika ligi ya msimu huu, baada ya kuichapa bao 1-0 katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Februari 2 mwaka huu katika Ligi Kuu soka Tanzania Bara.
Mbali na kuongoza ligi kwa jumla ya pointi 38 huku wakiwa na mechi nane mkononi, Yanga ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo.
Misimu mitatu iliyopita, Simba waliwahi kuitwa wazee wa Dozi, kutokana na kugawa dozi kwa kila klabu iliyokutana nayo. Walishinda mechi mfululizo hali iliyowaongezea heshima kwa kutwaa ubingwa wakiwa na pointi nyingi.
Kwenye msimu wa 2011/2012 Simba walicheza takriban michezo 10 bila kupoteza hata mmoja, kila timu iliyokuja ilipokea kichapo au sare ya aina yoyote ile. Simba walitawazwa Mabingwa wa msimu huo chini ya kocha Moses Basena kutoka Uganda.
Sababu ya kuleta maelezo hayo ni kuonyesha namna timu kubwa zinavyopewa majina makubwa kila zinavyofanya vizuri. Lakini zipo timu zinazotoka mikoani ambazo zinahitaji kusifiwa ili zipate mwanya wa kufanya vizuri.
Magazeti yote ya michezo kusipokuwepo na habari za Simba ama Yanga, hakuna mtu atakayenunua. Ni lazima kuwepo na rangi nyekundu ama njano katika kurasa za mbele ama za nyuma za magazeti ya michezo ama ya kawaida ndipo wanunuzi huvutiwa kununua.
Lakini kuna kitu kimoja, mara nyingi sifa wanazopata Simba ama Yanga zinawaelemea kiasi kwamba wanapopata mwanya wa kucheza mechi za kimataifa hawafanyi vizuri.
Kwa mwezi mzima sasa, Yanga wanahaha kutafuta dawa ya kuvuka kigingi cha klabu ya Al Ahly ya Misri katika Michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika. Kama Yanga ingekuwa inacheza soka la ushindani na si soka la kutaka kusifiwa, wasingekuwa na haja ya kuhangaika kutafuta mbinu mbadala kushinda mechi hiyo.
Hivyo ni vema klabu zetu zikaacha kufuata sifa za kwenye magazeti. Kuna haja ya timu hizi za Simba na Yanga kuwa na mipango enedelevu kuanzia kwenye ligi za ndani hadi katika mechi za kimataifa.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/simba-yanga-zimeshindwa-kuvuka-mipaka#sthash.s39KGNMP.dpuf
0 comments:
Post a Comment