Dar
es Salaam. Watanzania
23 waishio Afrika Kusini wamewekwa kwenye kambi maalumu ya Isipingo
nchini humo ili kupewa ulinzi wa maisha yao yaliyo hatarini kufuatia
mashambulizi yanayofanywa na wazawa dhidi ya wageni.
Watu
hao ambao ndiyo idadi ya Watanzania waliotambulika kuwa hatarini
nchini humo, wanatarajia kuwasili nchini muda wowote baada ya
Serikali ya Afrika Kusini kuridhia. Watakaorejea nchini ni Watanzania
21, wengine wawili wameomba kuendelea kubaki huko.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema
hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha katika vurugu zilizosababishwa na
chuki dhidi ya wageni, lakini wapo Watanzania watatu waliokufa nchini
humo kwa sababu nyinginezo.
Membe
aliwataja waliofariki kuwa ni Rashid Jumanne. Alisema Mtanzania huyu
alikuwa ni jambazi na aliuawa kilomita 90 kutoka mji wa Durban akiwa
kwenye harakati zake za unyang’anyi.
Mtu
wa pili alisema anaitwa Athman China. Alisema kijana huyu aliuawa kwa
kuchomwa kisu ndani ya gereza la West Hill. Membe alifafanua kuwa
China alifanya kosa la jinai akafungwa, na huko gerezani zikatokea
fujo za wafungwa. Kijana huyo alikufa baada ya kuchomwa kisu na
wafungwa wenzake.
Ally
Mohamed alikuwa ni kijana wa tatu kufa akiwa Afrika Kusini. Membe
alisema Mohamed alikuwa amelazwa hospitali huko Johanesberg kwa
maradhi ya kifua kikuu. Kijana huyo alifariki baada ya kuugua kwa
miezi miwili, na tayari mwili wake umewasili nchini kwa maziko.
“Kuna
habari zimesambaa mitandaoni kwamba Watanzania wamekufa huko Afrika
Kusini. Niweke wazi kuwa hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha kutokana
na vitendo vya chuki dhidi ya wageni. Mpaka sasa ni watu nane tu
ndiyo waliopoteza maisha,” alisema waziri huyo na kuongeza kuwa
watu hao wanatoka katika nchi za Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na
Swaziland.
Membe
alisema aliwasiliana na Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini, David
Mahlobo akamthibitishia kuwa hakuna Mtanzania yoyote aliyekufa. Pia,
alimwita balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ili aeleze zaidi
madhara yaliyojitokeza kwa Watanzania waishio Afrika Kusini.

0 comments:
Post a Comment