JUMAMOSI kutakuwa na fleva fulani hivi kwenye kabumbu. Mashabiki wa
Manchester United, Chelsea na Arsenal watashuhudia mechi ya Yanga na
Etoile du Sahel ya Kombe la Shirikisho ndani ya Uwanja wa Taifa kabla
ya kiama kingine cha England.
Wakitoka tu Taifa kuna vibarua viwili kwenye runinga zao siku hiyo
saa 1:30 usiku, Chelsea itakuwa inacheza na Man United katika Ligi
Kuu England wakati Arsenal itacheza na Reading katika nusu fainali ya
Kombe la FA. Ikaushie hiyo.
Yanga inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara mzimu
huu baada ya kuzizidi nguvu Simba na Azam, itakuwa na kibarua cha
kujitengenezea mazingira ya kusonga mbele kwenye raundi ya pili ya
Shirikisho dhidi ya timu ngumu ya Etoile ambayo ina bifu na Simba kwa
vile haijawalipa mamilioni ya usajili wa Emmanuel Okwi ingawa Fifa
imeamuru Mnyama alipwe.
Unajua Yanga ilichofanya? Baada ya kuzing’oa BDF ya Botswana na
Platinum ya Zimbabwe, sasa imeingia na gia mpya kwenye mechi nne
zilizobaki kufuzu hatua ya makundi wakianzia na mechi ya Jumamosi.
Katika mechi hizo nne Yanga imeweka mezani burunguti la Sh288 milioni
kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na inafuta rekodi ya Simba
ambayo imekuwa ikiwakejeli kwenye uwanja wa Taifa.
Simba inawakejeli Yanga kwa mambo mawili; inawaambia Yanga kwamba
wamezibahatisha BDF na Platinum na kwamba ndege yao ya mwisho Afrika
ni pale watakapoifuata Etoile, lakini pia inawaambia kwamba hawawezi
kufikia rekodi yao ya hatua ya makundi mwaka 2003.
Simba ilifuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka huo kwa
kuitoa Zamalek ya Misri ambao ni Waarabu kama ilivyo Etoile ya
Tunisia inayoanza na Yanga Dar es Salaam.
Lakini Yanga ni kama wameikomesha Simba kwani dau walilotenga kwenye
mechi hizo nne ni sawa na mishahara ya kulipa wafanyakazi wote wa
Simba kujumuisha wachezaji na makocha kwa miezi minne na chenji
inabaki.
Simba kwa mwezi inatumia Sh60 milioni kulipa mishahara, ambapo fungu
linaweza kulipa mishahara ya miezi minne.
Yanga hutumia Sh85milioni kulipa mshahara kwa mwezi.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Yanga imepitisha
bajeti ya kutumia si chini ya dola 40,000 (Sh72 milioni) katika kila
mchezo itakayocheza kuanzia sasa kimataifa kuiandaa timu kiufundi
pamoja na majukumu mengine ya nje ya uwanja ilimradi kusaka ushindi.
Mmoja wa vigogo wa Yanga amedokeza kwamba lengo lao ni kuingia kwenye
hatua ya makundi na kurejesha hadhi ya Yanga ambayo imekuwa
ikiipigania kwa misimu kadhaa ikiwa ni pamoja na kuajiri wataalamu
ghali kufikia hatua hiyo.
Etoile waja na rekodi
Yanga wanakutana na Etoile du Sahel ambayo haijawahi kushinda chini
ya mabao 7-0 inapocheza na timu ya Afrika Mashariki. Desemba mwaka
2006, Etoile ilitwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho ikiwa chini ya
kocha wa sasa Faouzi Benzarti kwa kuishinda klabu ya FAR Rabat ya
Morocco.
Lakini kwa mara ya kwanza Etoile ilicheza nchini Tanzania na Afrika
Mashariki kwenye raundi ya pili ya 16 bora dhidi ya Moro United
ambayo kwa wakati huo ilifahamika zaidi kama Chelsea ya Bongo.
Etoile iliishinda Moro kwa jumla ya mabao 7-1 ambapo katika mchezo wa
kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam Etoile walishinda 4-1, kisha
wakaishinda bao 3-0 kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa kule
Tunisia.
Kwenye takwimu za mtandao wa CAF zinaonesha kuwa klabu ya Etoile
haijawahi kucheza dhidi ya klabu nyingine ya Afrika Mashariki katika
miaka ya hivi karibuni zaidi ya Moro ambayo ilishajifia.
Kocha Mkuu wa Etoile, Faouzi Benzarti ameuambia mtandao mmoja wa
michezo wa Tunisia akisema: “Nilishawahi kwenda Tanzania mwaka 2006
na nilifanikiwa kuishinda moja ya timu ya nchi hiyo (Moro United)
ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikishiriki Shirikisho.
“Naamini
tutakapoenda Tanzania tutapata ushindi na tutakaporudi nyumbani pia
tutafanya viz

0 comments:
Post a Comment